Katika taarifa kwa taifa, makamu wa rais wa Venezuela Nicholas Marduro
ametangaza kufariki dunia kwa rais Hugo Chavez, 58, kufuatia kuugua muda
mrefu maradhi ya Saratani. Rais Chavez ametoweka katika hadhira ya nchi
hiyo kwa muda mrefu ambapo alikuwa anapokea matibabu nchi jirani ya
Cuba.
Alirejea , mjini Caracas mnamo Februari 18 kwa mara ya kwanza tangu
maradhi yake yamzidie ambapo alipelekwa hospitali ya kijeshi kuendelea
kupokea matibau. Hata hivyo maelezo zaidi hayakutolewa juu ya afya yake.
Waandamanaji waliandamana katika mji mkuu Caracas mwishoni mwa juma
wakidai kuwa watu wa Venezuela wanapaswa kupewa habari zaidi kuhusu afya
ya rais wao.
Bwana Chavez amekua uongozini nchini Venezuela kwa miaka 14 na
anatazamiwa kuleta mageuzi makubwa yaliyolenga zaidi kuimarisha maisha
ya raia wa pato la chini.
Ujumbe wa Jeshi
Taarifa kutoka kwa jeshi imesema kuwa wataendelea kuilinda hadhi ya nchi
na kuimarisha usalama. Pia jeshi limeahidi kuendelea kuwa waaminifu kwa
makamu wa rais Nicholas Marduro na wakatoa wito kwa raia kuwa watulivu.
Hugo Chavez
alijitosa katika siasa za Venezuela mnamo Februari 1992 akiwa luteni
katika jeshi. Aliongoza mapinduzi dhidi ya rais wa wakati huo Carlos
Andres Perez.
Lakini kutokana na kukosa usaidizi wa kutosha wa kijeshi, Chavez na wanamgambo wenzake walishindwa kunyakua madaraka hayo. Alikiri kushindwa na aliwekwa korokoroni.
Lakini kutokana na kukosa usaidizi wa kutosha wa kijeshi, Chavez na wanamgambo wenzake walishindwa kunyakua madaraka hayo. Alikiri kushindwa na aliwekwa korokoroni.
Aliingia uongozini baada ya ushindi mkubwa ulioviondosha vyama vya
kisiasa wakati huo. Katika kuapishwa kwake mnamo February 1999, Hugo
Chavez alitangaza wazi kwamba mipango yake ya mabadiliko ya kisiasa na
kiuchumi sio kampeni tu. Alitimiza ahadi yake na kuiongoza nchi hiyo
katika mabadiliko ambayo hayakuwahi kushuhudiwa katika muda wa miongo
kadhaa. Alibadili muundo wa bunge na kulifanya kuwa la kikatiba, ambalo
liliiunda katiba mpya baada ya kura ya maoni iliyoidhinishwa na 88% ya
wapiga kura.
Rais Chavez alitaifisha rasilmali ukiwemo utajiri wake mkubwa wa mafuta.
Sera kama hizi zilimfanya azozane na kampuni za kimataifa za mafuta,
lakini alipata uungwaji mkono mkubwa wa watu maskini.
Chavez na jamii ya kimtaifa
Kutokana na urafiki wake na viongozi wa mrengo wa kushoto kama vile rais
wa Cuba, Fidel Castro, ambaye walikuwa na uhusiano wa karibu aligongana
kidiplomasia na Marekani, ambayo ni mshirika wake mkuu wa kibiashara.
Chavez alipendwa nyumbani na wafuasi wake lakini alipingwa na baadhi ya
watu nchini humo na katika nchi za nje. Alionekana sio tu kama bingwa wa
jamii maskini lakini pia kama muingiliaji wa siasa za nchi jirani.
Katika miaka ya hivi karibuni alilenga kukabiliana na masuala ya ndani
ya Venezuela, kama uhalifu, kuinua uchumi wa nchi na kukabiliana na
rushwa.